Web Toolbar by Wibiya

Thursday, July 21, 2011

Madai ya ugaidi yazuia misaada Somalia

                                                                   hali halisi ya somalia
Huku maelfu ya watu nchini Somalia wakikabiliwa na tishio la kuangamia kufuatia athari za ukame na njaa, Rais mstaafu wa Ireland amekosoa baadhi ya nchi za Magharibi kwa kutoisaidia nchi hiyo.
Mary Robinson, ambaye amezuru somalia anasema nchi hizo zinasita kutoa msaada wa vyakula kwa raia wa Somalia kwa madai kuwa wengi wao ni magaidi.
Bi Robinson ambaye sasa ni kiongozi wa shirika la Oxfam, amekosoa nchi hizo muda mfupi tu baada ya Umoja wa Mataifa kutangaza kuwa Somalia inakabiliwa na baa la Njaa.
Amesema licha ya hali mbaya ya kibinadamu nchini humo, kasi ya kupokea misaada kwa walioathirika ni ya chini mno.
Umoja wa Mataifa umetangaza janga la njaa katika maeneo mawili ya kusini mwa Somalia ambayo kwa wakati huu yanakabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha zaidi ya nusu karne.
Umoja wa Mataifa unasema hali kwa watu waishio kusini mwa Bakool na Lower Shabelle imezorota kwa haraka sana. Hii ndio mara ya kwanza kwa nchi ya Somalia kukumbwa na janga la njaa katika kipindi cha miaka 19.
Na wakati huohuo, Umoja wa Mataifa na Marekani zimesema mashirika ya misaada yanahitaji hakikisho la usalama hasa kwa wafanyakazi wake kuwa hawatadhuriwa na makundi yalio na silaha na kuwa wataruhusiwa kuwafikia walengwa.
Al-Shabab, kundi linalohusishwa na al-Qaeda- ambalo linadhibiti maeneo makubwa ya kusini na kati mwa Somalia, lilikuwa limeyapiga marufu mashirika ya misaada ya kigeni kuingia katika maeneo yake mwaka 2009, lakini hivi sasa limeruhusu maeneo kadhaa kutembelewa.
Kote nchini Somalia nusu ya idadi ya raia kwa sasa wanakabiliwa na tatizo hilo kubwa ambapo watu wanaokisiwa kuwa milioni 2.8 wako katika eneo la kusini.
Taarifa ya ofisi ya mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya misaada kwa Somalia
Watu wanaokisiwa kuwa milioni 10 wanakabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika eneo la Afrika Mashariki katika kipindi cha nusu karne. Wasomali zaidi ya 166,000 inakisiwa wamekimbia nchi yao na kuingia Kenya na Ethiopia.
Ukame, mzozo na umasikini kwa mpigo zimechangia katika kuleta janga la njaa. watoto zaidi ya asili mia 30 wanautapia mlo na watoto wanne kati ya watoto elfu 10 wanakufa kila siku.
Inaaminika kuwa mzozo wa kivita unaoendelea hivi sasa unayatatiza mashirika ya misaada kuwafikia watu walio katika maeneo ya kusini yanayokaliwa na al-Shabab.
Hali ya hewa imekuwa mbaya katika maeneo hayo na kambi zimetatizika hasa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mapema wiki hii. Mvua hiyo ilisomba mabanda mengi ya wakimbizi hao wa ndani, wakimbizi hao walikuwa wanajenga mabanda yao wakitarajia kuwa mvua itanyesha katika meneo yanayokabiliwa na njaa.
Mwandishi wa BBC wa masuala ya Afrika Andrew Harding anasema kuwa maneno "janga la njaa" hayatumiwe sana na mashirika ya misaada na kuwa hii ndio mara ya kwanza tangu mwaka 1992 maneno hayo yametumiwa kueleza hali ya Somalia.

No comments: