Kundi la Al Shabaab limepinga tangazo la umoja wa mataifa kuwa Somalia inakabiliwa na baa la njaa na kuwa maelfu ya watu huenda wakaangamia.
Msemaji wa Al Shabaab Sheikh Ali Raage amesema kuwa tangazo hilo ni mbinu ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutoa misaada kuongeza chumvi kuhusu hali ilivyo Somalia.Sheikh Raage pia amebainisha kuwa sio mashirika yote ya kutoa misaada ambayo yataruhusiwa kusambaza vyakula nchini humo.
Kundi hilo linasema Somalia inakabiliwa na hali mbaya ya ukame na sio baa la njaa kama ilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa.
Umoja wa Mataifa unasema hali kwa watu waishio kusini mwa Bakool na Lower Shabelle imezorota kwa haraka sana. Hii ndio mara ya kwanza kwa nchi ya Somalia kukumbwa na janga la njaa katika kipindi cha miaka 19.
Kundi la Al Shabaab limesisitiza kuwa mashirika ambayo yalikuwa yamezuiwa kutekeleza shughuli zao nchini Somalia hayataruhusiwa kuingia nchini humo.
Hii ni kando na tamko lao wiki iliopita kuwa mashirika hayo yatakubaliwa kuingia katika maeneo wanayoyatawala kusini mwa Somalia.
"Hayo mashirika hayakubaliwa kuingia Somalia sio leo wala kesho. Yale ambayo tunayakubalia ni ambayo yamekuwepo nchini humu kwa muda wote huu. Tunapinga yale ambayo yanahusika na siasa na kupotosha watu wetu" Sheikh Raage alisema.
Msemaji huyo hakutaja majina ya mashirika hayo lakini yale yaliokuwa yamepigwa marufuku ni pamoja na shirika la chakula duniani (WFP), Care International na baadhi ya Umoja wa Mataifa.
Awali, Umoja wa Mataifa na Marekani yalitaka hakikisho la usalama hasa kwa wafanyakazi wake kuwa hawatadhuriwa na makundi yalio na silaha na kuwa wataruhusiwa kuwafikia walengwa.
Al-Shabab, kundi linalohusishwa na al-Qaeda- ambalo linadhibiti maeneo makubwa ya kusini na kati mwa Somalia, lilikuwa limeyapiga marufu mashirika ya misaada ya kigeni kuingia katika maeneo yake mwaka 2009, lakini hivi sasa limeruhusu maeneo kadhaa kutembelewa.
Kote nchini Somalia nusu ya idadi ya raia kwa sasa wanakabiliwa na tatizo hilo kubwa ambapo watu wanaokisiwa kuwa milioni 2.8 wako katika eneo la kusini.
Taarifa ya ofisi ya mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya misaada kwa Somalia
Ukame, mzozo na umasikini kwa mpigo zimechangia katika kuleta janga la njaa. watoto zaidi ya asili mia 30 wanautapia mlo na watoto wanne kati ya watoto elfu 10 wanakufa kila siku.
Inaaminika kuwa mzozo wa kivita unaoendelea hivi sasa unayatatiza mashirika ya misaada kuwafikia watu walio katika maeneo ya kusini yanayokaliwa na al-Shabab.
Hali ya hewa imekuwa mbaya katika maeneo hayo na kambi zimetatizika hasa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mapema wiki hii. Mvua hiyo ilisomba mabanda mengi ya wakimbizi hao wa ndani, wakimbizi hao walikuwa wanajenga mabanda yao wakitarajia kuwa mvua itanyesha katika meneo yanayokabiliwa na njaa.
Mwandishi wa BBC wa masuala ya Afrika Andrew Harding anasema kuwa maneno "janga la njaa" hayatumiwe sana na mashirika ya misaada na kuwa hii ndio mara ya kwanza tangu mwaka 1992 maneno hayo yametumiwa kueleza hali ya Somalia.
No comments:
Post a Comment